The Kingdom of Heaven

Directions

The Kingdom of Heaven MISSION - Preaching and teaching the good news of the Kingdom of Heaven.

10/24/2026

MUNGU MWENYEWE NDIYE ROHO YETU NA NDIYE UTUKUFU WETU NDANI MWETU

Sisi ni Hekau la Roho wa Mungu, na Roho wa Mungu anakaa ndani yetu. Sisi ni mwili wake, na Yeye ni Roho yetu mpya ndani mwetu.

Neno la Mungu linasema;

“Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?” (1 Wakoritho 3:16).

“Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu?” (1 Wakoritho 6:19).

“…..sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; k**a Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu” (2 Wakoritho 6:

Lakini pia Neno linasema Mungu ndiye Utukufu wetu.

“Wewe, BWANA, U…..Utukufu wangu….” (Zaburi 3:3).

“…..NA MUNGU WAKO atakuwa UTUKUFU WAKO” (Isaya 60:19).

“……NAMI NITAKUWA HUO UTUKUFU NDANI YAKE”(Zekaria 2:5).

“Kwa Mungu…..wangu, Na Utukufu wangu….” (Zaburi 62:7a).

“….BWANA…..ni taji ya UTUKUFU…..kwa…..watu wake” (Isaya 28:5).

Maana yake Utukufu wetu ni wa ki-Mungu na sio wa ki-binadamu.

Hivyo sisi kuwa na Roho wa Mungu ndiye kuwa na utukufu wetu wa Mungu ndani mwetu. Na kuishi kwa Roho ya Mungu ya Utukufu ndio kunatupa kuudhihirisha utukufu wa Mungu katika maisha yetu.

Hii ndio sababu kwa nini Mungu ametuambia tuishi kwa Roho, tuenende kwa Roho, tuombe kwa Roho, tuabudu kwa Roho, na tufanye mambo mengine yote pia kwa Roho. K**a maisha yetu ni ya kufanya mambo yote kwa Roho ya Mungu, maana yake Roho ya Mungu (Kristo) hakika imekuwa Roho yetu, nasi tunapaswa kuishi kwa Roho hii mpya yetu tuliyopewa na kudhihirisha utukufu wetu.

Na k**a Mungu ndiye Roho yetu na Utukufu wetu, maana yake kumpenda Mungu katika Kristo Yesu, ndio kujipenda wenyewe. Huwezi ukaamua kutokujipenda mwenyewe kwa kutokumpenda Mungu aliye Roho na Utukufu wako katika maisha yako.

Maana kutokumpenda Mungu ni kutokujipenda mwenyewe, maana Mungu ndio Roho yetu na Utu wetu au Nafsi yetu mpya ndani mwetu sisi tuliompokea. Jipende mwenyewe kwa KUIPENDA Roho na Nafsi yako ambayo ni Roho ya Mungu. Upende Utukufu wako kwa kuipenda Roho ya Mungu ambayo ndio utukufu wako. Umebarikiwa sana. Halleluya!!

10/19/2026

UTUKUFU WA MUNGU NDIO UTUKUFU WETU NA SIO UTUKUFU WA BINADAMU

“Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu……Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba” (Ufunuo 1:26-27).

Tuliumbwa kwa mfano wa Mungu na sio kwa mfano wa mwanadamu. Tuliumbwa ili tuwe k**a Mungu na sio tuwe k**a wanadamu.

Hivyo Mungu kutuumba kwa mfano wake ili tuwe k**a Yeye, maana yake utukufu wetu Mungu alioukusudia kwetu ni utukufu wake na sio utukufu wa kibinadamu.

Anasema Mungu pia sehemu nyingine, kuwa Yeye ndiye utukufu wetu.

“Wewe, BWANA, U…..Utukufu wangu….” (Zaburi 3:3).

“Jua halitakuwa nuru yako tena wakati wa mchana, Wala mwezi hautakupa nuru kwa mwangaza wake; Bali BWANA atakuwa nuru ya milele kwako, NA MUNGU WAKO atakuwa UTUKUFU WAKO” (Isaya 60:19).

“Kwa maana mimi, asema BWANA, nitakuwa ukuta wa moto kuuzunguka pande zote, NAMI NITAKUWA HUO UTUKUFU NDANI YAKE”(Zekaria 2:5).

“Na mji ule hauhitaji jua wala mwezi kuuangaza, kwa maana UTUKUFU WA MUNGU HUUTIA NURU, na TAA yake [au UTUKUFU wake] ni Mwana-Kondoo” (Ufunuo 21:23).

“Kwa Mungu wokovu wangu, Na Utukufu wangu….” (Zaburi 62:7a).

“Katika siku ile BWANA wa majeshi atakuwa ni taji ya UTUKUFU, na kilemba cha uzuri, kwa mabaki ya watu wake” (Isaya 28:5).

“Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao…..” (Yohana 17:22a).

Maandiko yote hayo yanasema Mungu ndiye utukufu wetu, maana yake Utukufu wetu sio wa binadamu bali ni wa Mungu mwenyewe.

Tukiwa na Roho wa Mungu ndani yetu, ndio tunakuwa na Utukufu wa Mungu. Maana (1 Petro 4:14) inasema Roho wa Mungu ndani mwetu ni 👉🏽 “Roho wa utukufu na wa Mungu.”

Anaitwa pia Baba wa utukufu. 👉🏽 “Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, BABA WA UTUKUFU…..” (Waefeso 1:17).

Pia sehemu nyingine Neno linasema;

“Siri ile iliyofichwa tangu zamani zote na tangu vizazi vyote, bali sasa imefunuliwa kwa watakatifu wake; ambao Mungu alipenda kuwajulisha jinsi ulivyo UTAJIRI wa UTUKUFU wa SIRI HII katika Mataifa, nao ni KRISTO NDANI YENU, TUMAINI LA UTUKUFU” (Wakolosai 1:26-27).

Hiyo☝️ndio siri iliyofichwa toka Mwanzo, kwamba Kristo ndani yetu ni tumaini la Utukufu, au Kristo ndani yetu ni tegemeo au tarajio la Utukufu.

Ukiwa unaye Kristo (Roho wa Mungu) sasa, tambua kuwa unaye Roho wa Utukufu wa Mungu ndani yako, unaye UTUKUFU WA MUNGU sasa ndani yako.

Na ukianza kuishi kwa nguvu ya Roho hiyo ya Utukufu, Utukufu wa Mungu utaanza kudhihirika katika maisha yako.

KRISTO NDANI YAKO, TUMAINI LA UTUKUFU.

“ambaye kwa yeye [Kristo Yesu] tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo mnasimama ndani yake; na kufurahi katika tumaini la utukufu wa Mungu” (Warumi 5:2).

K**a wewe unaye Kristo ndani yako, wewe ni Mtoto au Mwana wa Mungu na una utukufu wa Mungu sasa na sio wa kibinadamu. Wewe haufanani sasa na wanadamu wengine, bali wewe unafana sasa na Mungu.

Muundo mkuu wa kibiblia unavyopaswa kuwa;

👉🏽 Mungu Mwenyewe — Utukufu Wetu (Zaburi 3:3; Isaya 60:19).

👉🏽 Yesu Kristo — Utukufu wa Mungu Uliofunuliwa (Yohana 1:14; 2 Wakorintho 4:6).

👉🏽 Kanisa — Linabadilishwa ili Kuakisi Utukufu Wake (Yohana 17:22; 2 Wakorintho 3:18).

👉🏽 Uumbaji Mpya — Umejaa Utukufu Wake (Habakuki 2:14; Ufunuo 21:23).

Hivyo usijafananishe wa wanadamu wengine tena, maana Mungu hakutuumba tuwe k**a wanadamu wengine, bali tuwe k**a Yeye.

Hivyo siku zote jifananishe na Mungu tu, jifananishe na Yesu tu. Usijifananishe wa watu au wanadamu wengine kabisa. Mungu akubariki sana. Amina!!

10/14/2026

UTUKUFU WA MUNGU WA MWISHO KATIKA KANISA SIKU HIZI ZA MWISHO UTAKUWA MKUU SANA NA KUIJAZA DUNIA YOTE

“Utukufu wa mwisho wa nyumba hii utakuwa mkuu kuliko utukufu wake wa kwanza, asema BWANA wa majeshi…..” (Hagai 2:9a).

Ndugu zangu, kuna umuhimu mkubwa sana kwa ajili ya kila mmoja wetu kujiandaa kwa ajili ya utukufu wa Mungu mkuu katika siku hizi za mwisho.

Toka Mwanzo Mungu alikusudia kuishi katikati ya wanadamu na kujidhihirisha kwao. Ndio maana Mungu alipowaumba watu, akawaweka kwenye bustani yake ya Edeni na kuishi pamoja nao humo.

“Kisha wakasikia sauti ya BWANA Mungu, akitembea bustanini wakati wa jua kupunga…..” (Mwanzo 3:8).

Na hata baada ya dhambi bado tunaona Mungu anaendelea katika kusudi lake hilo la kutaka kukaa katikati ya watu wake.

Hii ndio sababu Mungu alimwambia M***a;

“Nao na wanifanyie patakatifu; ili nipate kukaa kati yao” (Kutoka 25:8).

Katika Biblia yote unaona hili kusudi la Mungu linaendelea mpaka katika kitabu cha Ufunuo.

Ziko hatua tano za Ufunuo wa Mungu wa kuurejesha huu ulimwengu katika kusudi lake la kuujaza ulimwengu huu na Utukufu wake k**a vile mbinguni kulivyo.

HATUA YA 1.

Utukufu katika hema katikati ya Israel;

(Kutoka 40:34–35) inasema;

“Ndipo lile wingu likaifunikiza hema ya kukutania, na huo utukufu wa BWANA ukaijaza maskani. Wala Musa hakuweza kuliingia hema la kukutania, kwa sababu lile wingu lilikaa juu yake, na huo utukufu wa BWANA ukaijaza maskani.”

Na Utukufu huo uliokuwa uko katika hema hiyo, ulikuwa unaonekana kwa watu wote

(Mambo ya Walawi 9:23–24) inasema;

“Kisha Musa na Haruni wakaingia ndani ya hema ya kukutania, kisha wakatoka nje, na kuwabarikia watu; na huo utukufu wa BWANA ukawatokea watu wote. Kisha moto ukatoka hapo mbele za BWANA……watu wote walipouona huo moto wakapiga kelele wakainama kifudifudi.”

HATUA YA 2.

Utukufu katika hekalu la Mfalme Sulemani katikati ya Israel;

(1 Wafalme 8:10–11) inasema;

“Ikawa, makuhani walipotoka katika patakatifu, nyumba ya BWANA ikajaa wingu; hata makuhani hawakuweza kusimama ili kufanya huduma yao, kwa sababu ya wingu lile; kwa kuwa nyumba ya BWANA ilikuwa imejaa utukufu wa BWANA.”

Hili linafanana moja kwa moja na Kutoka 40:34–35. Katika hema, utukufu ulijaza hema; katika hekalu, utukufu ulijaza hekalu na kudhihirika.

HATUA YA 3.

Utukufu umefunuliwa ndani ya Kristo k**a hekalu halisi la Mungu;

(Yohana 1:1,14) inasema;

“Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu k**a wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.”

(Yohana 2:19–21) inasema;

“Yesu akajibu, akawaambia, Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha. Basi Wayahudi wakasema, Hekalu hili lilijengwa katika muda wa miaka arobaini na sita, nawe utalisimamisha katika siku tatu? Lakini yeye alinena habari za hekalu la mwili wake.”

(Wafilipi 1:19; 2:9) inasema;

“Kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae. Maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili.”

(Waebrania 1:3) inasema;

Yesu ni mng’ao wa utukufu wa Mungu na chapa ya nafsi ya Mungu.

Mwana wa Mungu anafunua utukufu wote wa Baba na pia anasema Yeye ndio Hekalu halisi ambalo Mungu alilikusudia utimilifu wa utukufu wake wote ukae ndani yake.

HATUA YA 4.

Utukufu huo unaanza kuongezeka na kuijaza dunia kwa kupitia Kanisa k**a hekalu la Mungu hilo Kristo linalokua na kuongezeka

(Waefeso 2:29–22) inasema;

“Basi tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu. Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni. Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana. Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho.”

(Waefeso 3:21) inasema;

“Mungu atukuzwe awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu (yake) itendayo kazi ndani yetu; naam, atukuzwe katika Kanisa na katika Kristo Yesu hata vizazi vyote vya milele na milele.”

Anasema hapo, Mungu huyo katika UTIMILIFU wake wote wa utukufu, anakaa na anafanya mambo ya ajabu mno kutokea ndani yetu sisi hekalu lake, na pia anatukuzwa katika Kanisa na katika Kristo Yesu hata vizazi vyote vya milele na milele.

HATUA YA 5.

Utukufu wa Mungu utajazwa duniani kote

(Habakuki 2:14) inasema;

“Kwa maana dunia itajazwa maarifa ya utukufu wa BWANA, k**a maji yaifunikavyo bahari.”

(Isaya 11:9) inasema;

“…..dunia itajawa na kumjua BWANA, k**a vile maji yanavyoifunika bahari.”

Hesabu 14:20-21 inasema pia;

“BWANA akasema…..hakika yangu, k**a niishivyo, tena k**a dunia hii nzima itakavyojawa na utukufu wa BWANA.”

(Ufunuo 21:22-23) inasema;

“Nami sikuona hekalu ndani yake; kwa maana Bwana Mungu Mwenyezi na Mwana-Kondoo, ndio hekalu lake. Na mji ule hauhitaji jua wala mwezi kuuangaza, kwa maana utukufu wa Mungu huutia nuru, na taa yake ni Mwana-Kondoo.”

Kusudi la Mungu linaelekea kwenye kuujaza utukufu wake duniani kote, na hatimaye utukufu wake kuangaza katika uumbaji wake wote mpya.

Na utukufu huu wa Mungu ulio katika hekalu (Kanisa) lake, unazidi kuongezeka kadri Kanisa linapozidi kukua zaidi na kupanuka duniani na kuijaza dunia, ndivyo Mungu atazidi kuijaza dunia yote na utukufu wake.

Tutaendelea kuona vizuri zaidi hilo kadri tutavyokuwa tunaendelea kujifunza haya huku mbele. Usikose kufuatilia hili somo kila tunapotuma. Mungu awabariki sana. Amina!!

10/11/2026

UTUKUFU MKUU WA MUNGU KATIKA SIKU HIZI ZA MWISHO

Ndugu zangu wapendwa,

Ninamshukuru Mungu kwa ajili ya neema hii tena aliyotupatia ya kuendelea kujifunza pamoja. Nimekuwa kimya kwa muda mrefu kwa kusudi la kupata muda na nafasi pia ya kumtafuta Bwana zaidi na kupokea zaidi toka kwa Bwana yale aliyokusudia kuendelea kutupatia katika siku hizi za mwisho.

Katika kipindi hiki Mungu ameendelea kunionyesha na kunisemesha mambo mengi sana. Mojawapo ya mambo aliyoendelea kunisemesha, ni watu wake kujiandaa kwa ajili ya Utukufu Mkuu katika siku hizi za mwisho.

Siku hizi za mwisho ni siku za kudhihirisha Utukufu Mkuu wa Mungu alioukusudia kuudhihirisha katika ulimwengu katika siku hizi za mwisho, na sio siku za kumwogopa mpinga Kristo na dhiki kuu na kujiandaa kutoroka duniani.

Siku za mwisho hazipaswi kueleweka tu kuwa ni siku za mpinga Kristo, giza, mitikisiko, hofu, udanganyifu, dhiki na mateso, bali pia ni siku za Mungu kumiminwa Roho wake, kuufunua zaidi utukufu Wake, kudhihirisha nguvu Zake, kuhukumu uovu duniani, na kudhihirisha utawala Wake kupitia watu Wake. Biblia inajumuisha hali hizi zote mbili.

Watu wengi wa Mungu wametiwa hofu kwa sababu ya kusikia habari mbaya za mambo ya upande mmoja tu wa giza yatakayokuwepo, bila ya kujua mambo mazuri zaidi yatakayokuwepo katika upande wetu wa nuru. Na wengi kwa sababu ya kusikia habari hizo za upande mmoja tu wa giza wametiwa hofu na wanatamani tu kukimbia duniani.

Neno la Mungu linasema,

“Maana, tazama, giza litaifunika dunia, Na giza kuu litazifunika kabila za watu; Bali BWANA atakuzukia wewe, Na utukufu wake utaonekana juu yako. Na mataifa wataijilia nuru yako, Na wafalme kuujia mwanga wa kuzuka kwako” (Isaya 60:2-5).

Neno hapo☝️linatuonyesha wazi kuwa katika siku za mwisho ni kweli “giza litaifunika dunia,” lakini pia anasema, “utukufu wake utaonekana juu yako. Na mataifa wataijilia nuru yako, Na wafalme kuujia mwanga wa kuzuka kwako.”

Unaweza kuona hapo mwenyewe, kipi kitakuwa na nguvu kati ya giza la siku za mwisho au nuru na utukufu wa Mungu wa siku hizi za mwisho? Unaona wazi, nuru au utukufu huo wa Mungu utakuwa mkuu sana kushinda giza litakalokuwepo katika siku hizi za mwisho.

Hivyo hiyo inatupa kuona siku za mwisho ni siku za udhihirisho wa utukufu wa Mungu zaidi na sio giza. Hivyo hatuhitaji kuogopa habari za giza la siku hizi za mwisho hata kidogo. Tunatakiwa kujiandaa tu kwa ajili ya kudhihirisha utukufu huo mkuu wa Mungu katika siku hizi za mwisho.

Hivyo usiogope ndugu yangu siku hizi za mwisho, kwa sababu sisi ni Nuru na Utukufu wa Ulimwengu, Mungu anaenda kushinda hilo giza lote na kuliondoa ulimwenguni kupitia sisi, na utukufu wake kuujaza ulimwengu wote.

Hivyo tujiandae ndugu zetu kutumiwa na Yesu kuudhihirisha utukufu huo wake mkuu katika siku hizi za mwisho. Mungu akubariki sana. Amina!!

08/18/2026

URAIA WETU SIO WA DUNIANI KATIKA NCHI YEYOTE ILE, BALI URAIA WETU NI WA MBINGUNI KATIKA KRISTO.

“Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo; atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake” (Waefeso 3:20-21).

Ndugu zetu, sisi tuliozaliwa mara ya pili na Roho Mtakatifu wa Mungu, uraia wetu ni wa Mbinguni na sio duniani.

K**a vile;

👉🏽 Watanzania ni raia wa Tanzania
👉🏽 Wakenya ni raia wa Kenya
👉🏽 Waganda ni raia wa Uganda
👉🏽 Wamarekani ni raia wa Marekani

Vivyo hivyo pia na;

👉🏽 Wakristo ni raia wa mbinguni ndani ya Kristo

Biblia inasema, sisi tuko ndani ya Kristo, na ndani ya Kristo tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uhai wetu (Matendo 17:28). Maana yake Kristo ni nchi na ni makao ya watu wa Mungu katika ulimwengu wa Roho, k**a vile nchi zingine zilivyo katika dunia hii.

Hivyo sisi kuitwa wa-kristo maana yake sisi ni raia wa nchi inayoitwa Kristo. Na nchi hii inayoitwa Kristo ndio nchi ya mbinguni. Kuwa ndani ya Kristo ndio kuwa ndani ya nchi ya mbinguni.

Lakini Kristo sio tu ni nchi yetu mpya, bali pia ndio mwili wetu mpya wa Roho. Kuwa ndani ya Kristo, ni kuwa ndani ya mwili mpya wa Roho wa mbinguni. Kuwa katika Kristo, maana yake tumevua sasa mwili wa nyama (wa duniani) na tumevaa mwili mpya wa Roho (wa mbinguni).

“Katika yeye mmetahiriwa kwa tohara isiyofanyika kwa mikono, kwa kuuvua mwili wa nyama, kwa tohara ya Kristo” (Wakolosai 2:11).

Tulipoletwa duniani Mungu alitupatia mwili wa duniani (mwili ya nyama), na alipokuja kutuokoa na kututoa duniani akatupatia mwili mpya wa mbinguni (mwili ya Roho).

“Hupandwa mwili wa asili; hufufuliwa mwili wa roho. Ikiwa uko mwili wa asili, na wa roho pia uko. Ndivyo ilivyoandikwa, Mtu wa kwanza, Adamu, akawa nafsi iliyo hai; Adamu wa mwisho ni roho yenye kuhuisha.

Lakini hautangulii ule wa roho, bali ule wa asili; baadaye huja ule wa roho. Mtu wa kwanza atoka katika nchi, ni wa udongo. Mtu wa pili atoka mbinguni.

K**a alivyo yeye wa udongo, ndivyo walivyo walio wa udongo; na k**a alivyo yeye wa mbinguni, ndivyo walivyo walio wa mbinguni. Na k**a tulivyoichukua sura yake yule wa udongo, kadhalika tutaichukua sura yake yeye aliye wa mbinguni.

Ndugu zangu, nisemayo ni haya, ya kuwa nyama na damu haziwezi kuurithi ufalme wa Mungu; wala uharibifu kurithi kutokuharibika” (1 Wakoritho 15:44-50).

Anasema hapo juu;

“Mtu wa kwanza atoka katika nchi, ni wa udongo. Mtu wa pili atoka mbinguni.

K**a alivyo yeye wa udongo, ndivyo walivyo walio wa udongo; na k**a alivyo yeye wa mbinguni, ndivyo walivyo walio wa mbinguni,”

maana yake, k**a “Mtu wa pili atoka mbinguni” ndivyo hivyo pia na sisi “walio wa mbinguni” tumetokea mbinguni.

07/22/2026

MAKUHANI WA KIFALME WANAHUDUMU KATIKA HEKALU LA MUNGU LA MBINGUNI NA SIO DUNIANI

“…..ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi” (Ufunuo 5:9b-10).

“Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme…..” (1 Petro 2:9).

Maneno hayo ☝️yanasema Yesu alitununua sisi kwa damu yake na kutufanya kuwa MAKUHANI WA KIFALME kwa Mungu.

Sisi k**a Makuhani wa Kifalme wa Agano Jipya la KIROHO au la ROHONI, tunahudumu katika hekalu la ROHONI la Mbinguni na sio katika hekalu la MWILINI la duniani.

Yesu k**a Kuhani wetu Mkuu, anahudumu katika hekalu la Mbinguni na sio la duniani.

Neno linasema;

“Tunaye kuhani mkuu wa namna hii, aliyeketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Ukuu mbinguni, mhudumu wa patakatifu, na wa ile hema ya kweli, ambayo Bwana aliiweka wala si mwanadamu” (Waebrania 8:1-2).

Katika hekalu hilo Kuhani wetu Mkuu anapohudu, ndipo na sisi makuhani tulio chini yake tunahudumu pamoja naye hapo.

Kumbuka Yeye na sisi tumeungana na kuwa Roho moja naye. Kumbuka Yeye ni kichwa na sisi ni mwili wake, Kichwa + Mwili = Mtu mmoja aliye kamili. Kumbuka pia sisi tuko ndani yake, hivyo alipo Yeye ndipo tulipo na sisi, anapohudumu Yeye ndipo na sisi hapo hapo tunapohudumu pamoja naye.

Hivyo k**a Yeye “ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Ukuu mbinguni”, ndivyo na sisi tumeketi pamoja naye hapo. Na k**a Yeye ni “mhudumu wa patakatifu, na wa ile hema ya kweli, ambayo Bwana aliiweka wala si mwanadamu,” na sisi pia tu wahudumu pamoja naye katika hema hiyo hiyo.

Hapo ndipo sisi k**a makuhani wa kifalme tunapotakiwa kuwepo kiroho na kutoa huduma hapo za kiroho mbele za Mungu kwanza, na kutokea hapo kwenda kwa watu ulimwenguni kote. Mungu awabariki sana. Amina!!

07/20/2026

KUKAA NA KUISHI NA MUNGU KATIKA MAKAZI YAKE YA MBINGUNI SASA TUKIWA DUNIANI

“BWANA Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai. BWANA Mungu akapanda bustani upande wa mashariki wa Edeni, akamweka ndani yake huyo mtu aliyemfanya” (Mwanzo 2:7-8).

Mungu alipomuumba mwanadamu alimweka katika Bustani ya Edeni, hakumweka mahali pengine popote pale. Bustani ya Edeni katika sehemu zingine katika maandiko, inaitwa bustani ya Mungu (Ezekieli 28:13;31:8-9), inaitwa Sayuni (Isaya 51:3), inaitwa mlima Mtakatifu wa Mungu (Ezekieli 28:14,16).

Inaitwa pia “Paradiso” (Ufunuo 2:7) na “Yerusalemu mpya” (Ufunuo 22:2) kwa sababu ya mti wa uzima uliokuwa ndani yake. Inaitwa pia Mbinguni Yerusalemu mpya iko mbinguni. Kwa hivyo Mungu alipomuumba mwanadamu alimweka katika bustani yake, katika mlima wake Mtakatifu, katika Paradiso, ndani ya mbinguni, ili tuishi huko tukiwa duniani.

Mungu alimweka mwanadamu katika bustani yake, katika makao yake mwenyewe ili aweze kuishi naye mahali Yeye anapoishi mbinguni akiwa duniani. Hilo ndilo Mungu alilolikusudia tangu mwanzo, kuishi pamoja na watu wake mahali anapoishi Yeye tukiwa duniani. Mungu hakukusudia watu waishi nje ya Yeye alipokuwa anaishi. Ndio maana mtu kabla ya kutenda dhambi, Mungu hakukusudia kumtoa mtu katika bustani yake hiyo.

Mtu alipotenda dhambi, ndipo Mungu alipomtoa katika bustanini yake, katika makao yake, katika Paradiso yake - mbinguni kwake, na kuanza kuishi duniani tu bila ya kuwa mbinguni. Yesu alipokuja kulipa gharama ya dhambi za watu waliofanya, na kutufanya tena wenye haki, kusudi lake ni kuturudisha sisi tena katika bustanini yake, katika makao yake tena, mbinguni kwake tena ili tuweze kuishi pamoja naye tena huko tukiwa duniani.

Hilo ndilo Yesu alilofanya na kulikamilisha katika ulimwengu wa Roho, alipokufa na kufufuka na kuketishwa mbinguni kwa ajili yetu (Waefeso 2:4-6). Tayari tumesharudishwa kwa Mungu sasa katika bustani yake, katika makao yake - Mbinguni, ili tuishi kutokea mbinguni duniani. Tayari tumesharejeshwa mbele zake mahali Yeye alipo. Tumesharejeshwa katika uwepo wake. Yeye alipo sasa ndipo na sisi pia tulipo sasa. Hili tayari limeshafanyika katika Kristo, si kana kwamba tunasubiri lifanyike katika siku zijazo.

K**a hili tayari limeshakuwa katika Kristo, basi tunahitaji kuamini na kuanza kuishi humo sasa pamoja na Yeye katika Roho, huku tukiwa duniani. Tayari tumesharudishwa mbinguni sasa katika bustani yake, na tunaishi pamoja naye sasa katika bustani yake k**a alivyokusudia tangu mwanzo.

Si kwamba tuko njiani tunakwenda huko sasa, bali tayari tumeshafika sasa katika mlima Sayuni, na mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu wa mbinguni. Neno linasema, “Bali ninyi mmeshafika katika mlima Sayuni, na mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu wa mbinguni, na majeshi ya malaika elfu nyingi, mkutano mkuu na kanisa la wazaliwa wa kwanza walioandikwa mbinguni, na Mungu mwamuzi wa watu wote, na roho za watu wenye haki waliokamilika, na Yesu mjumbe wa agano jipya….” (Waebrania 12:22-24).

Hapo ndipo Mungu anasema, hayo ndio makazi yetu sisi na Yeye. Neno linasema, “Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, umewekwa tayari, k**a bibi-arusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe. Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao” (Ufunuo 21:2:3).

07/09/2026

MUNGU ALIKUSUDIA WANA WAKE KUWA NDIO WATAWALA WA ULIMWENGU

“Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa sura yetu, kwa mfano wetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi” (Mwanzo 1:26).

Katika mstari wetu wa ufunguzi, watu waliye na sura na mfano wa Mungu ni wana wake. Na wana wake ndio hao Mungu amesema hapo alikusudia wawe watawala wa ulimwengu, na sio watu wasio wana wake.

Utawala huu Mungu aliowapatia wana wake katika ufalme wake wa rohoni, ulikuwa ni wa ulimwengu wa rohoni kwanza na pia katika ulimwengu wa mwilini. Hii ndio maana unaona Yesu alisema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani” (Mathayo 28:18), kwa ajili yetu sisi.

Na hiyo ndio mamlaka ya jina la Yesu aliyopewa kwa ajili yetu. Neno linasema, “Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba” (Wafilipi 2:9-11).

Hiyo ☝️ndio mamlaka yetu, Yesu aliyopewa kwa ajili yetu wana wa Mungu, na akatupatia sisi mamlaka hiyo ili tuweze kutawala vitu vyote vya mbinguni, duniani, na chini ya nchi. Hiyo ndio mamlaka tunayotakiwa kuitumia kutawala vitu vyote vya mbinguni, duniani, na chini ya nchi, ili kusimamia mapenzi yake yaweze kutimia katika maeneo yote hayo. Mungu awabariki sana nyote. Amina!!

07/06/2026

NJIA PEKEE YA KUTUMIA KUIKOMBOA TANZANIA NI NJIA YA MUNGU NA SIO YA DUNIA

“Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo” (Matendo 4:12).

Ndugu zangu, njia pekee na ya kweli ya kuikomboa Tanzania ni njia ya Mungu na sio ya dunia. Katika mstari wetu wa ufunguzi, Neno la Mungu linasema, “hakuna wokovu (ukombozi) katika mwingine awaye yote, zaidi ya katika Yesu tu.” Anasema, “kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.”

Hivyo kutafuta kuiokomboa Tanzania bila ya kumtumia Yesu, na uwezo wake, na kutumia njia zake, hatuwezi kuikomboa Tanzania kutoka kwa adui. Yesu ndiye pekee tuliyepewa na Baba kuja kutukomboa kutoka kwa adui Shetani. K**a vile kila mtu bila Yesu hakuna wokovu, ndivyo hivyo pia kila Taifa ua nchi bila Yesu hakuna wokovu.

“Baba amemtuma Mwana kuwa Mwokozi wa ulimwengu” (1 Yohana 4:14).

Na Yesu alipokuja kuuokoa ulimwengu kutoka kwa adui, hakutumia njia za duniani za kivita za kimwili, bali alitumia njia za Mungu za kiroho. Maana adui Shetani ni wa rohoni na sio wa mwilini. Vivyo hivyo na Tanzania pia, adui wa kweli wa Tanzania ni wa rohoni na sio wa mwilini. Hivyo kuikomboa Tanzania tunapaswa kutumika njia za Roho wa Mungu za rohoni na sio njia za roho ya Shetani za mwilini.

Neno linasema, “Kwa maana vita vyetu sisi si juu ya damu na nyama (wanadamu); bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho” (Waefeso 6:12).

“Lakini mimi nikitoa pepo kwa Roho wa Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia” (Mathayo 12:28).

K**a Mungu anatuambia, vita vyetu sio dhidi ya wanadamu bali dhidi ya roho za giza, hivyo vita yetu sio ya kimwili bali ni ya kiroho. Wanadamu wanatumiwa tu na roho za giza kutenda mabaya kwa wengine, hivyo hao sio maadui zetu bali ni roho hizo za giza zinazowatumikisha hao watu kufanya hayo mabaya. Hii ndio sababu Yesu alisema, “Baba wasamehe hao” watu walionisubisha “maana hawajui walitendalo.” Halafu akaenda akamshughulikia Shetani kuzimu na kumshinda na kutoka kuzimu akiwa amepata ushindi wa wokovu.

Hivyo tusiwachukie wanadamu hata hao tunaoona k**a maadui zetu. Hii ndio sababu kwa nini Yesu alisema, “Lakini nawaambia ninyi…..Wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wawachukia ninyi, wabarikieni wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wawaonea ninyi” (Luka 6:27-28).

“Maana mkiwapenda wale wawapendao ninyi, mwaonyesha fadhili gani? Kwa kuwa hata wenye dhambi huwapenda wale wawapendao. Nanyi mkiwatendea mema wale wawatendeao mema, mwaonyesha fadhili gani? Hata wenye dhambi hufanya vivyo hivyo. Na mkiwakopesha watu huku mkitumaini kupata kitu kwao, mwaonyesha fadhili gani? Hata wenye dhambi huwakopesha wenye dhambi, ili warudishiwe vile vile.

Bali wapendeni adui zenu, tendeni mema, na kukopesha msitumaini kupata malipo, na thawabu yenu itakuwa nyingi; nanyi mtakuwa wana wa Aliye juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru, na waovu. Basi, iweni na huruma, k**a Baba yenu alivyo na huruma” (Luka 6:32-36).

Hivyo tusifanye vita na wanadamu kwa sababu hao sio maadui wetu, bali tufanye vita na Shetani pamoja na roho zake za giza katika ulimwengu wa rohoni na kumshinda na kupata ushindi wa kuikomboa nchi na Taifa.

Na Maombi ni mojawapo ya silaha kubwa sana tunayotakiwa kutumia kupigana vita na Shetani. Tuombe sana ndugu zetu Ili kumshughulikia adui kwa umoja na kumshinda. Mungu awabariki sana. Amina!!

07/05/2026

YESU ANASEMA: HUWEZI KUMTOA SHETANI KWA KUMTUMIA SHETANI

Yesu; “aliletewa mtu mwenye pepo, kipofu, naye ni bubu; akamponya, hata yule bubu akanena na kuona” (Mathayo 12:22).

“Lakini Mafarisayo waliposikia [Yesu amemponya mtu mwenye pepo], walisema, Huyu hatoi pepo, ila kwa Beelzebuli mkuu wa pepo” (Mathayo 12:24).

Yesu akawaambia;

“Awezaje Shetani kumtoa Shetani?” (Marko 3:23).

Maana yake huwezi kumtoa pepo (Shetani) kwa kumtumia mkuu wa pepo (Shetani).

Yesu akawaambia pia ni kwa nini hatuwezi kumtoa Shetani kwa kumtumia Shetani. Akasema;

“Kila ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, hufanyika ukiwa; tena mji au nyumba yo yote ikifitinika juu ya nafsi yake, haitasimama. Na Shetani akimtoa Shetani, amefitinika juu ya nafsi yake; basi ufalme wake utasimamaje?” (Mathayo 12:25-26).

Halafu akawaambia;

“Mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, je! Wana wenu huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo hao ndio watakaowahukumu” (Mathayo 12:27).

Yesu alisema hilo kutuonyesha kuwa, wana wa Shetani ndio hutoa pepo kwa mkuu wa pepo, lakini Yeye hatoi pepo kwa mkuu wa pepo.

Halafu akawapa jibu, akawaambia;

“Lakini mimi nikitoa pepo kwa Roho wa Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia” (Mathayo 12:28).

Yesu hapo aliwaambia namna Yeye anayotoa pepo (Shetani) - akasema kwa Roho wa Mungu. Na akasema Yeye anapotoa Shetani kwa Roho Mungu, ndio mjue ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia au umeshakuja ili kuwapatia haki yenu mliyoibiwa, mliyokuwa mnaitafuta.

Na mwisho Yesu akasema;

“Ama awezaje mtu kuingia ndani ya nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuviteka vyombo vyake, asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu? Ndipo atakapoiteka nyumba yake” (Mathayo 12:29).

Maana yake hutuwezi kwenda kwa Shetani mwenye nguvu, pasipo kuwa na nguvu kubwa zaidi ya Roho wa Mungu kuliko yake na kumfunga kwanza Shetani, na ndipo tutaweza kuteka nyumba yake.

Hatuwezi kumtoa Shetani mwenye nguvu juu ya Tanzania k**a hatutatumia nguvu za Roho wa Mungu kumfunga na kuichukua Tanzania toka kwake.

Yesu ametuonyesha hapo kuwa, hakuna nguvu ya ki-binadamu inayoweza kumshinda Shetani. Yesu mwenyewe amesema hakutumia nguvu ya kibinadamu au ya mkuu wa pepo. Hakuna nguvu ya chuki, hasira, maandamano, fujo, uharibifu, uchomaji vitu, vurugu, uuaji au roho za giza zinaweza kumshinda Shetani. Kwa sababu hivyo vyote ni vya Shetani, vyote hivyo ni nguvu ya Shetani.

Yesu alisema Shetani hawezi kumtoa Shetani. Hivyo tusitumie nguvu hizo za Shetani kumtoa Shetani aliyeiba haki za watanzania, bali tutumie Roho wa Mungu kumtoa Shetani. Hivyo maandamano hayawezi kutoa roho ya Shetani juu ya Tanzania. Ni nguvu za Mungu tu ndio zinaweza. Hivyo ndugu zangu msiende kupoteza maisha bure kwenye maandamano bila faida yeyote. Huu sio uoga nawapa, huu ni ukweli nawapa. Sikilizeni tafadhali nawaomba sana.

Tutumie mamlaka ya kiti cha enzi cha Roho ya Yesu Kristo, mamlaka ya jina la Yesu kumtoa Shetani kwa njia ya maombi. Tutumie upendo wa Roho, utii kwa Roho, unyenyekevu kwa Roho, utakatifu wa Roho, mamlaka ya Roho, nguvu za Roho, na silaha zingine zote za Mungu. Kwa njia hiyo tu pekee ndio tutapata ushindi. Mungu atusaidie sana kuelewa. Amina!!

Address

Willmar, MN

Website

Alerts

Be the first to know and let us send you an email when The Kingdom of Heaven posts news and promotions. Your email address will not be used for any other purpose, and you can unsubscribe at any time.

Shortcuts

Share